Fowadi wa Ubelgiji Divock Origi akihutubia wanahabari Juni 13, 2014 nchini Brazil. Picha/AFP
Baada
ya Divock Origi kusaidia Ubelgiji kufuzu kwa kundi H kwenye dimba la
dunia kule Brazil, mchezaji huyo amesema anajivuna kuwa Mkenya licha ya
kuliwakilisha taifa jingine kwenye soka ya kimataifa.
RIO De JANEIRO, Brazil.
BAADA ya
Divock Origi kusaidia Ubelgiji kufuzu kwa kundi H kwenye dimba la dunia
kule Brazil, kwa bao la kipekee alilotia kimyani dhidi ya Urusi hapo
Jumapili, mchezaji huyo alisema anajivuna kuwa Mkenya licha ya
kuliwakilisha taifa jingine kwenye soka ya kimataifa.
Mshambuliaji huyo wa
klabu ya Lille, Ufaransa , mwenye asili ya Kenya ambaye ana uraia wa
Ubelgiji, alipachika bao hilo la pekee kunako dakika ya 88 baada ya
kuingia kama nguvu mpya mahala pa Romelu Lukaku, na kisha kuandaliwa
pasi murwa na kiungo wa Chelsea, Eden Harzad.
“Pamoja na
kwamba naichezea taifa la Ubelgiji katika soka ya kimataifa, sio siri
kwamba naijivunia kuwa Mkenya kwani ndio mizizi halisi ya asili yangu.
Bao lile nimelielekezea Wabelgiji wote kwa kunikuza na vile vile Wakenya
ambalo ndilo taifa la wazazi wangu,” Origi alinukuliwa.
Bao hilo la dakika za
majeruhi za mchuano huo ndio iliyoiwezesha Ubeljiji kufuzu kwa hatua ya
timu 16 bora kwenye kundi H kwa kuzoa jumla ya alama sita. Hii ni baada
pia ya kuandikisha ushindi mwingine kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya
Algeria waliowalaza 2-1. Sasa wamesalia na mechi moja dhidi ya Korea
Kusini na hata ikiwa watapoteza, tayari wamefuzu kwa duru ya pili.
Kwenye mechi nyingine ya kundi hilo, Korea Kusini waliotoka sare ya 1-1
na Urusi kwenye mechi ya awali, walilimwa 4-2 na Algeria.
Baada ya
kuhangaishwa sana na Urusi pamoja na kucheza kwenye joto kali, Origi
aliipata nafasi ya kuvurumsha kombora nzito hadi kimyani zikiwa
zimesalia dakika mbili mchezo kuisha, kufuatia mashambulizi ya kaunta
alipopokea pasi nzuri yake Hazard kutoka kushoto mwa kisanduku cha
wapinzani.
Mahojiano
Straika huyo
mwenye umri wa miaka 19, ni mwanawe Mike Okoth, mshambuliaji na nahodha
wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.
Akifanyiwa
mahojiano na kituo hicho cha BBC kuhusu hatua ya mwanawe kuichezea
Ubelgiji badala ya Kenya, mkongwe Okoth alikuwa na haya ya kujibu.
“Baada ya
ushauri wa kutosha, aliamua kuichezea Ubeljiji kwa kuzingatia masuala
mengi; kama vile usimamizi mzuri wa kandanda nchini humo taofauti na
ilivyo Kenya. Isitoshe ni Ubelgiji ambapo alikuza kipaji chake
akiichezea katika viwango vyote kuanzia soka ya wachezaji wasiozidi umri
wa miaka 16, 17, 19 na sasa 21,” alisema.
Kingine
kikubwa kilichomfanya kukataa kuiwakilisha Kenya ni kiwango cha soka cha
Kenya ambacho kipo chini na vile vile hatua ya Ubelgiji kufuzu mara kwa
mara kushiriki dimba la dunia tofauti na Kenya.
“Isitoshe
baada ya mimi kuichezea Harambee Stars kwa muda mrefu, ninfahamu bayana
changamoto chungu nzima zinazoikumba na kwa sababu Kenya haijulikani ni
lini itafuzu kwa dimba la dunia, nilimshauri mwanangu kuichagua
Ubelgiji,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment