Dodoma.Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali haijafuta daraja sifuri katika
matokeo ya mitihani taifa ya shule za sekondari na kwamba ilichokifanya
ni kuondoa mrundikano wa madaraja.
Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Magige alitaka kufahamu kama kushusha madaraja ni
suluhisho la kuwaokoa vijana waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato
cha nne mwaka jana.
Mapema katika swali lake la msingi, Magige,
alitaka kufahamu kama Serikali ina mkakati wa kuanzisha mpango maalumu
hasa wa ufundi kwa wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato
cha nne mwaka jana.
Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali.
“Tumeongeza madaraja ili kuwatambua watoto,
kulikuwa na mrundikano katika daraja moja. Serikali haijafuta division
ziro na wala hakuna division V, ipo division I, II,III, IV na ziro kama
kawaida,” alisema.
Alisema uamuzi wa kushusha madaraja, hauna lengo
la kuwaokoa wanafunzi wanaofanya vibaya na badala yake, unalenga katika
kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.
Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.
Alisema kulikuwa hakuna ufuatiliaji wa maendeleo
ya mwanafunzi kama kanuni inavyosema kuwa lazima kuwe na ufuatiliaji wa
asilimia 50 kwa 50 .
Alisema kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa alama 50
katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi na katika mtihani ya
kumaliza shule asilimia 50.
Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.
Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kujibu swali hilo, Spika wa Bunge,
Anne Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka bungeni kauli ya waziri
kuhusiana na suala hilo.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema
Kuhusu wanafunzi waliofanya vibaya mwaka jana
katika mitihani yao, Mulugo alisema Serikali haitaanzisha mpango maalumu
wa ufundi kwa vijana hao.
Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.
Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho. CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment